KENYA

Maseneta nchini Kenya kujadili mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi

Bunge nchini Kenya
Bunge nchini Kenya Wikipedia

Maseneta nchini Kenya watakutana siku ya Jumatano kujadili na kuyapigia kura mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2017.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya bunge la Kitaifa kufanikiwa kuibadilisha sheria hiyo wiki iliyopita.

Mabadiliko hayo yanairuhusu Tume ya Uchaguzi kutumia mfumo wa kawaida, kuwatambua wapiga kura na kujumuisha matokeo, ikiwa mfumo wa eletroniki utagoma kufanya kazi.

Wiki iliyopita, wabunge wa upinzani walisusia mjadala huo lakini wabunge wa serikali wakaupitisha kwa sababu ya wingi wao bungeni lakini pia baada ya mvutano uliosababisha hata wabunge kupigana.

Upinzani unadai kuwa serikali imeungana mkono mabadiliko hayo ili kuiba kura za urais, madai ambayo serikali imekanusha.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ameipa serikali siku nane, kuja katika meza ya mazungumzo kujadili suala hili la sivyo, kutakuwa na maandamano ya nchi nzima tarehe 4 mwezi Januari mwaka 2017.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki, na viongozi wengine wa dini pia wamejitokeza na kumtaka rais Uhuru Kenyatta kutokubali mabadiliko hayo na kutoa nafasi ya kuwepo kwa mazungumzo ya kisiasa.