SUDAN KUSINI

Rais Kiir awataka raia wa Sudan Kusini kusameheana

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir REUTERS/Jok Solomon

Rais wa Sudan Salva Kiir, amewataka raia wa nchi yake kusameheana kuelekea mwaka mpya wa 2017.

Matangazo ya kibiashara

Kiir amesisistiza kuwa ni kupitia tu kwa msamaha ndio nchi yake itapata amani ya kudumu baada ya kupitia wakati mgumu wa vita tangu ilipoanza kujitawala mwaka 2011.

“Nazifahamu sana changamoto zinazowakabili,” alisema rais Kiir.

“Naelewa sana mateso mnayotumia, na kusababisha mgogoro wa uchumi bila kusahau kushuka thamani kwa Pauni yetu,” aliongeza.

Aidha, kiongozi huyo amesema hakuna haja tena ya kuwauwa raia wasiokuwa na hatia kama ilivyoshuhudiwa mwaka 2016.

Kiongozi wa Kanisa  Katoliki nchini humo  Paulino Lokudu Loro katika ujumbe wa Krismasi, ameitaka serikali ya Juba kuheshimu haki za binadamu.

“Lazima haki za binadamu ziheshimiwe mwaka mpya wa 2017,” amesema Askofu Mkuu Loro.

Wito huu unakuja baada ya Kiir wiki iliyopita, kutoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa.

Kiongozi wa upinzani na waasi, Riek Machar anaishi nchini Afrika Kusini kwa sasa baada ya kuondoka jijini Juba baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya vikosi vyake na vile vya Kiir mwezi Agosti.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa huenda kukatokea kwa machafuko ya kikabila nchini humo ikiwa, pande zote mbili hazitakutana na kufikia mwafaka wa kisiasa.