KENYA

Maseneta nchini Kenya wakubaliana kupitiwa upya kwa mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi

Bunge nchini Kenya
Bunge nchini Kenya Wikipedia

Maseneta nchini Kenya, wamekubaliana kuwa mjadala wa mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi ushughulikiwe katika Kamati ya Haki za Binadamu na sheria.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu umekuja baada ya Maseneta kukutana kwa dharura kujadili mabadiliko hayo yaliyopitishwa na bunge la kitaifa wiki iliyopita na kuzua mjadala wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Mabadiliko hayo yanaipa nafasi Tume ya Uchaguzi kutumia njia mbadala ya kuwatambua na kujumuisha matokeo ya Uchaguzi Mkuu ikiwa mfumo wa Ki-eletroniki utagoma siku ya kupiga kura.

Spika wa Baraza la Senate Ekwe Ethuro amesema, Kamati hiyo itatoa nafasi kwa mashirika ya kiraia, viongozi wa dini na wadau wengine kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo.

“Waheshimiwa Maseneta,naagiza kuwa Kamati ya sheria na haki za binadamu ishughulikie mswada huu, kwa mujibu wa Katiba na kanuni zetu kuanzia hivi leo,"

"Lakini pia naagiza kuwa Kamati hii iwahusishe wadau wote wa uchaguzi na wananchi na kuzingatia yale yote yanazunguziwa kuhusu mswada huu,” alisema Ethuro

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Amos Wako ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, amesema kamati yake itafanya kazi yake bila upendeleo wowote.

“Kamati inahisi kuwa suala hili ni la dharura sana na linastahili kutafutiwa ufumbuzi wa haraka. Natoa wito kwa umma kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao mbele ya kamati, ni kazi ngumu lakini tutajaribu kadiri ya uwezo wetu,” alisema Wako.

Upinzani unasema mabadiliko hayo yanaipa nafasi serikali kuiba kura, madai ambayo serikali inakanusha.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametangaza kuwa kutakuwa na maandamano ya nchi nzima tarehe 4 mwezi Januari ikiwa mabadiliko hayo yatakuwa yametupiliwa mbali.

Hata hivyo, huenda maandamano hayo yasifanyike ikiwa Kamati ya Senate itakuja na mapendekezo yatakayokuwa yamekubaliwa na pande zote mbili za kisiasa.