BURUNDI

Rais wa Burundi asema yuko tayari kuwania muhula mwingine 2020 ikiwa katiba itafanyiwa marekebisho

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza AFP PHOTO / MARCO LONGARI

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, amesema ikiwa katiba ya nchi yake itafanyiwa marekebisho na kuondoa vipengele kuhusiana na mihula ya uchaguzi atagombea tena kiti cha urais ifikapo mwaka wa 2020 

Matangazo ya kibiashara

Akijibu maswali ya wanahabari na raia katika kipindi cha moja kwa moja kilichorushwa kwenye radio ya taifa hilo, rais Nkurunziza amesema suala si kuwepo wa mihula bali ni kuwepo kwa uongozi na kwamba kama katiba itamruhusu kugombea hatosita kufanya hivyo mwaka wa 2020 kutokana na utashi wa raia.

Hayo yanajiri wakati huu kukiwa na mjadala nchini Burundi ili kutafuta ufumbuzi wa masuala ya mizozo inayotokana na uchaguzi ambayo huibuka mara kwa mara nchini Burundi huku washiriki wengi wakipendekeza vipengele vinavyozungumzia mihula ya rais vifutwe ambapo upande wa serikali tayari umeunda kamati inayohusika na kupendekeza marekebisho ya katiba kabla ya mswada wa sheria kupelekwa bungeni.

Mbali na suala hilo rais Nkurunziza amesema kuwa ikiwa hadi mwisho wa mwezi januari mwaka 2017 majeshi ya Burundi yanayohudumu katika kikosi cha AMISOM nchini Somalia hayatakuwa yamelipwa malimbikizo ya mshahara wao,watarejeshwa nchini na kuufungulia mashtaka Umoja wa Afrika.