TANZANIA-EAC

Tanzania: Jamii yasikitishwa wasanii kutumia dawa za kulevya

Wakati idadi ya wasanii wanaotumia dawa za kulevya nchini Tanzania ikiendelea kuongezeka huku vijana wengi nchini humo na ukanda wa Afrika mashariki wakiona ndio suluhu ya kumaliza matatizo yao, Serikali nchini Tanzania imeanzisha msako dhidi ya wauzaji na waingizaji wa dawa za kulevya nchini humo.

Msanii wa Tanzania Chid Benz anayetajwa kuathiriwa na dawa za kulevya.
Msanii wa Tanzania Chid Benz anayetajwa kuathiriwa na dawa za kulevya. YouTube
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii ya Serikali nchini Tanzania, imekuja, baada ya hivi karibuni wimbi la wasanii wanaotumia dawa za kulevya likiendelea kuongezeka na kutishia mustakabali wa vijana ambao wamo kwenye tasnia hiyo.

Hivi karibuni mmoja wa wasanii waliowahi kuvuma sana kwa aina ya muziki anaoufanya Chid Benzi, hali yake imeendelea kuzorota kutokana na kuathirika pakubwa na dawa za kulevya, maarufu nchini Tanzania kama “unga”.

Msanii huyu licha ya kuwahi kupelekwa katika kituo maalumu kinachotoa huduma kwa watu walioathirika na dawa za kulevya, bado baada ya kutoka, alirejea tena katika kutumia Unga, hali inayomfanya sasa kukosa usaidizi wa aina yoyote kumnusuru.

Mbali na Chid Benz, yuko pia msanii wa kike aliyewahi kuvuma nchini Tanzania na Afrika Mashariki, maarufu kama Rehema Chalamila “Ray C” aliyewahi kupokea msaada kutoka kwa aliyekuwa rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete ambaye alilipia gharama za matibabu yake, lakini nae baada ya kutoka huko alirejea kutumia unga.

Mbali na wasanii hawa, wamo pia wasaani wengine wengi wanaoimba, kuigiza na sanaa nyingine ambao nao wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya ambazo bila kujua wanajikuta wanashindwa kuacha na kuathirika pakubwa.

Wanajamii nchini humo wameonesha kuchukizwa na ongezeko la vijana maarufu kujitumbukiza kwenye matumizi ya dawa hizo, ambazo wanasema kamwe haziwezi kumaliza matatizo yao bali zaidi ni kuongeza mzigo kwa jamii na familia zao.

Baadhi ya wazazi waliozungumza na idhaa hii, wamesema kuwa, mbali na kuwa jukumu kubwa la kudhibiti vijana kujitumbukiza kwenye matumizi ya dawa linaanzia katika ngazo ya familia, wanasema Serikali pia inao mchango mkubwa katika kuwakabili waingizaji na wauzaji wa dawa hizi.

Kamishna wa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya nchini Tanzania ACP Mihayo Msikhela, amesema kuwa kitengo chake kimeanzisha msako maalumu dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya pamoja na wale wauzaji wadogo, ili kuhakikisha wanazuia mianya yote inayotumiwa na wauzaji hao kuzifikiza dawa hizo nchini.

Kamishina Msikhela, amekiri kuwa janga la dawa za kulevya nchini Tanzania ni kubwa na juhudi za makusudi zinaendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha wahusika wa biashara hii haramu wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya ndani ya nchi wa Tanzania Mwigulu Nchemba, amesema hali hiyo haikubaliki na kwamba wao kama wizara tayari wameanza mikakati madhubuti kuhakikisha wanawanusuru vijana hawa dhidi ya matumizi ya unga, ikiwa ni pamoja na kuwasaka wauzaji wenyewe.

Kwa upande wao viongozi wa dini nchini humo, mbali na kuitaka jamii kubadili mtazamo kuhusu familia, wanasema ni jukumu la kila mtu kuhakikisha wanawasaidia vijana kiimani ili kuwaondolea dhana kuwa unga ndio suluhu ya matatizo na badala yake watafutiwe vitu vingine vya kufanya ambavyo vitawaepusha na utumiaji wa dawa.

Kwa mujibu wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya nchini Tanzania, kiwango cha dawa zinazoingia na kukamatwa kimepanda kutoka kilo tatu za dawa aina ya Heroin mwaka 2008 hadi kilo 265.54 mwaka 2011 na kile nne za dawa aina ya Cocaine hadi kufikia kilo 128.30 mwaka huo huo.

Tatizo hili hata hivyo haliko pekee nchini Tanzania kwani hata kwenye nyingine za Afrika mashariki hasa pwani ya Mombasa nchini Kenya, vijana wengi wamekuwa wakijiingiza katika matumizi ya unga.

Nchi za Afrika Mashariki zimekuwa zikitumika kama sehemu ya kupitishia dawa kwenda maeneo mengine ya dunia ambapo dawa hizo zimekuwa zikitokea nchi za Afghanstan, India, Iran na Pakistan na kupelekwa nchi kama China, Japan, Afrika Kusini, Marekani na nchi zingine za Ulaya.

Aidha ripoti zinaonesha kuwa katika kila watu 100 barani Afrika, watu 8 wanatumia bangi na hivyo kuifanya bangi kuongoza kwa matumizi makubwa Afrika na zaidi matumizi ya bangi yapo nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.

Dawa nyingine zinazoongoza kwa matumizi makubwa Afrika ni pamoja na dawa aina ya Heroin ambapo katika watu 1,000 watu 3 wanatumia dawa hiyo na Cocaine inashika nafasi ya tatu kwa matumizi makubwa.