KENYA-MADAKTARI

Kenya: Serikali yapendekeza nyongeza ya asilimia 40 kwa madaktari

Serikali ya Kenya, imetangaza kutoa nyongeza ya mshahara ya asilimia 40 kwa madaktari waliogoma nchini humo, ili kumaliza mgomo ambao umedumu kwa zaidi ya mwezi sasa.

Mmoja wa madaktari ambao wanashiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi.
Mmoja wa madaktari ambao wanashiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Pendekezo hili la Serikali lilitangazwa katika ikulu ya Mombasa, baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa saa kadhaa kati ya wawakilishi wa madaktari na rais Uhuru Kenyatta.

Pendekezo hili, sasa litashuhudia madaktari wanaolipwa mshahara wa chini ukipanda hadi kufikia shilingi za Kenya laki 196,898 kutoka shilingi laki 140,244 mashahara waliokuwa wakilipwa awali.

Taarifa ya ikulu imesema kuwa malipo haya yamejumuisha marupurupu mengine ya mshahara yanayotolewa kwa madaktari kulinga na kazi wanazofanya na ngazi waliyopo.

Mkutano huu umefanyika baada ya madaktari hao kutoa wito kwa rais Kenyatta kama kiongozi wa juu wa nchi, kuingilia kati mgomo huo ili kuumaliza.

Baada ya saa sita za mazungumzo kati ya madaktari, katibu mkuu wa chama cha madaktari wa meno Ouma Oluga, amesema wameridhishwa na hatua iliyochukuliwa na rais.

"Hatujafikia makubaliano yoyote lakini tunamshukuru rais kwa kuitisha mkutano huu." alisema Oluga.

"Ameonesha kuguswa na madai yetu na tulizungumza kwa kina, tumekuwa na mazungumzo mazuri na shirikishi na tumekubaliana kuwa bado kuna changamoto," alisema.

Madaktari hao sasa watakutana katika mabaraza yao kuzungumzia pendekezo hili la Serikali na ikiwa wasitishe mgomo wao au la, tangazo ambalo sasa linasubiriwa kwa hamu na gamu na raia wa Kenya ambao wameendelea kuathirika kutokana na kuendelea kwa mgomo huu.

Madaktari hawa wanataka nyongeza ya asilimia 300 kama ilivyowahi kukubaliwa na Serikali.