Jeshi la Uganda kufanya operesheni dhidi ya wafugaji kutoka Kenya
Imechapishwa:
Jeshi la Uganda UPDF, limepiga kambi katika eneo la Karamoja mpakani na Kenya tayari kwa operesheni ya kuwaondoa wafugaji wa jamii ya Turkana kutoka nchi jirani.
Operesheni hii imeagizwa kufanyika na Mkuu wa Jeshi nchini humo, Edward Katumba Wamala, baada ya wafugaji hao kutuhumiwa kuendelea kuwauzia silaha wakaazi wa eneo la Karamoja na hivyo kuendelea kuhatarisha hali ya usalama.
Wafugaji hao pia wamekuwa wakituhumiwa kuvuka mpaka hadi nchini Uganda na mifugo yao wakiwa wamebeba silaha licha ya kuonywa na serikali ya Uganda kuacha kutembea na silaha.
Jeshi la Uganda linasema Operesheni hii itaanza wakati wowote ili kuimarisha usalama katika eneo la Karamoja.
Wafugaji hao kutoka nchini Kenya wapatao 50,000 huvuka kwenda Uganda kwenda kutafuta maji na nyasi kwa mifugo yao.
Mbali na Uganda, wizi wa mifugo kati ya jamii za wafugaji za Waturkana, Wasamburu na Wapokot nchini Kenya umeendelea kuzua ukosefu wa usalama katika Kaunti ya Baringo.
Licha ya Kenya kuwa na kitengo maalum cha kukabiliana na wizi wa mifugo, hakijafanikiwa kikamilifu kuzuia wizi huu wa mifugo.
Mwaka 2012, maafisa wa polisi waliuawa baada ya kushambuliwa na wezi wa mifugo katika eneo la Baragoi katika Kaunti ya Samburu.