KENYA

Upinzani nchini Kenya warejea Mahakamani kupinga mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi

Raïla Odinga, kiongozi wa upinzani nchini Kenya
Raïla Odinga, kiongozi wa upinzani nchini Kenya Reuters / Luc Gnago

Muungano wa upinzani nchini Kenya CORD, umerejea Mahakamani jijini Nairobi, kusikiliza kesi iliyowasilisha kuitaka Mahakama kutangaza kikao cha dharura cha bunge la taifa kilichofanyika mwezi Desemba mwaka uliopita kuifanyia marekebisho sheria ya Uchaguzi kuwa haramu.

Matangazo ya kibiashara

Mawakili wa upinzani, wakiongozwa na Seneta James Orengo, wanasema kuwa kikao hicho kilichoitishwa na Spika wa kitaifa Justin Muturi, hakikufanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Aidha, upinzani unasema wabunge wake hawakushauriwa mapema kuhusu kikao hicho ambacho wabunge wa serikali walifanikiwa kuiifanyia marekebisho sheria hiyo baada ya wabunge wa upinzani kuondoka bungeni.

Upinzani unadai kuwa, serikali inataka kutumia mabadiliko hayo kuiba kura wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu, madai ambayo serikali inapinga na kusema mabadiliko hayo yalipendekezwa na Tume ya Uchaguzi.

Mabadiliko hayo ambayo pia yalipitishwa katika Bunge la Senate wiki iliyopita, baada ya Maseneta wa upinzani na serikali kushindwa kukubaliana, yanaipa mamlaka Tume ya Uchaguzi kutafuta njia mbadala ya kuwatambua wapiga kura na kujumuisha matokeo ikiwa, mfumo wa eletroniki utagoma.

Upinzani unasema kama njia mbadala itatumika, basi iwe ni ya eletroniki, ili kuzuia wizi wa kura.

Hatima ya sheria hiyo, ipo mikononi mwa rais Kenyatta ambaye ana uwezo wa kuitia saini au kuikataa wakati huu wanaharakati na wadau mbalimbali wa kisiasa wakimtaka kuyakataa mabadiliko hayo.

Wanasiasa wa upinzani wanatarajiwa kuwa na kikao cha pamoja siku ya Jumatano jijini Nairobi, kuchukua msimamo wa pamoja baada ya mabadiliko hayo kupitishwa na Bunge la Senate.