Rais Museveni apangua uongozi wa jeshi, amteua mwanawe kuwa mshauri wake
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefanya mabadiliko katika uongozi wa jeshi nchini humo.
Imechapishwa:
Mkuu wa Majeshi Jenerali Katumba Wamala, ameondolewa katika wadhifa huo na sasa atakuwa Waziri wa Kazi.
Rais Museveni amemteua, Meja Jenerali David Muhoozi ambaye amekuwa Mkuu wa jeshi la nchi kavu, kuwa Mkuu mpya wa jeshi la UPDF.
Mtoto wa rais Museveni Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba naye ameondolewa katika wadhifa wa kuwa Kamanda wa vikosi maalum vinavyomlinda rais, na sasa ni mshauri maalum wa baba yake.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa, huenda mabadiliko haya hasa dhidi ya Kainerugaba, yanahusiana na madai ya mpango wa rais Museveni kumwandaa kumwachia madaraka atakapostaafu.
Hata hivyo, Jenerali Kainerugaba amekuwa akikanusha madai hayo na kusema kuwa yeye, sio mwanasiasa na hajawahi kufikiria kuwa rais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.