KENYA

Serikali nchini Kenya yatishia kuwafuta kazi Madaktari wanaogoma

Serikali nchini Kenya imewataka Madaktari wanaogoma kurudi kazini kufikia siku ya Jumatano wiki hii la sivyo wafutwe kazi.

Mmoja wa madaktari ambao wanashiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi.
Mmoja wa madaktari ambao wanashiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya Madaktari hao ambao wamekuwa wakigoma tangu mapema mwezi Desemba mwaka 2016, kukataa pendekezo la serikali kuwaongezea mshahara kwa asilimia 40.

Madaktari hao wameendelea kusisitiza kuwa, hawatarudi kazini hadi pale serikali itakapotekeleza mkataba waliokubaliana na serikali mwaka 2013, kuwaongezea mshahara kwa asilimia 300.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini humo Peter Munya, amezitaka serikali za Kaunti nchini humo kuwa tayari kuanza zoezi la kuwaajiri Madaktari wapya ikiwa wanaogoma hawatarudi kazini.

Wiki iliyopita, rais Uhuru Kenyatta alikutana na wawakilishi wa Madaktari hao katika Ikulu ya Mombasa na kuwaomba kukubali nyongeza ya mshahara ya asilimia 40, pendekezo ambalo lilikataliwa na wahudumu hao wa afya.

Waziri wa afya Cleopa Mailu amesema licha ya kuzungumza na viongozi wa Madaktari hao, kuwasihi ili kuwahimiza  zaidi ya Madktari 3,000 wanaogoma kurudi kazini ili kuwapa huduma wagonjwa wanaoteseka, juhudi zao hazijafanikiwa.

Hata hivyo, mgomo huo haujaathiri huduma za afya katika Kaunti za Marsabit, Bomet, Nakuru, Lamu, Garissa na Tana River kaunti ambazo zimefanikiwa kuwarejesha Madaktari kazini.

Mahakama Kuu jijini Nairobi siku ya Jumanne, iliamuru kukamatwa kwa wawakilishi wa Madaktari hao baada ya kutofika Mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili.