Upinzani nchini Kenya waunda muungano mpya wa kisiasa
Imechapishwa: Imehaririwa:
Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya wamezindua muungano mpya wa kisiasa unaofahamika kama NASA, kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti mwaka huu.
Muungano huo sasa una kazi kubwa ya kumtafuta mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya muungano huo dhidi ya rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee atakayetetea wadhifa wake.
Vyama vilivyoungana ni pamoja na ODM kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Wiper kinachoongozwa na aliyekuwa Makamu wa rais Kalonzo Musyoka, FORD Kenya kinachoongozwa na Seneta Moses Wetangula, AMANI kinachoongozwa na Musalia Mudavadi ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa rais, miongoni mwa vyama vingine.
Mbali na uzinduzi huo, wanasiasa hao wametoa wito kwa wafuasi wao kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha kama wapiga kura kuanzia siku ya Jumatatu wiki ijayo.
Kuhusu sheria mpya ya Uchaguzi iliyotiwa saini na rais Uhuru Kenyatta, viongozi wa muungano huo mpya wamesema hawayatambui mabadiliko ya sheria hiyo.
Seneta Wentangula amesema ikiwa, sheria hiyo itaendelea kuwepo baada ya zoezi la kujiandikisha kumalizika, wafuasi wa upinzani watakuwa na maandamano ya nchi nzima kutaka sheria hiyo kutotumiwa wakati wa uchaguzi.
Sheria hiyo ya Uchaguzi inaipa Tume ya Uchaguzi mamlaka ya kutafuta mfumo mbadala wa kuwatambua na kujumuisha matokeo, ikiwa mfumo wa eletroniki utagoma, mfumo ambao wanasiasa hao wanasema serikali inapinga kuiba kura kutumia sheria hii mpya.
Baada ya mkutano huu wa upinzani, chama cha Jubilee nacho kitakutana siku ya Ijumaa jijini Nairobi kupanga mikakati yake.