KENYA-SIASA

Upinzani nchini Kenya unakutana kuunda muungano mpya wa kisiasa

Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya wanakutana jijini Nairobi, kutangaza muungano mpya wa kisiasa unaovileta pamoja idadi kubwa ya vyama vya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga REUTERS/Goran Tomasevic
Matangazo ya kibiashara

Kumekuwa na mikakati ya kuunda muungano wa pamoja unaofahamika kama National Super Alliance (Nasa) kuvileleta pamoja vyama vyote vya upinzani, kupambana na chama cha Jubilee cha rais Uhuru Kenyatta, ambaye anatetea nafasi yake katika Uchaguzi huu.

Muungano huo wa NASA unavileta pamoja vyama vinne ambavyo ni ODM, Wiper, FORD Kenya na Amani National Congress. Mbali na muungano huu mpya, kumekuwa na muungano wa CORD ambao umekuwa ukiviunganisha vyama vya ODM, WIPER na FORD Kenya.

Baada ya kutangazwa rasmi kwa muungano huu wa kisiasa, kibarua kinachosalia ni cha kumtafuta atakayepeperusha bendera ya kuwania urais chini ya muungano huo mpya kati ya Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Moses Wetangula na Musalia Mudavadi.

Mbali na muungano huu, wanasiasa hao pia wanatarajiwa kutangaza msimamo wao kuhusu sheria mpya ya Uchaguzi iliyotiwa saini na rais Uhuru Kenyatta.

Upinzani unasema, sheria hiyo kuipa Tume ya Uchaguzi kutafuta mbinu mwafaka itakayokuwa mbadala ikiwa, mfumo wa Eletroniki  kuwatambua wapiga kura na kujumuisha matokeo utagoma.

Wanasiasa hao wanadai, sheria hii mpya ilibadilishwa makusudi ili kumsaidia rais Kenyatta kushinda tena Uchaguzi Mkuu, madai ambayo serikali imekanusha na kusema mapendekezo hayo yalipendekezwa na Tume ya Uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi imetangaza kuwa, itaanza kuwasajili wapiga kura wapya kuanzia wiki ijayo.