UGANDA-TANZANIA

Kampuni ya Marekani yapewa kandarasi ya kuthathmini njia ya kusafirisha mafuta

Bomba la mafuta
Bomba la mafuta thenerveafrica.com

Uganda na Tanzania zimeipa kandarasi kampuni ya Marekani ya Gulf Interstate Engineering, kuthathmini na kuandaa eneo ambalo bomba la kusafirisha mafuta litapita kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Habari la Uingereza Reuters, ambalo limeona kandarasi hiyo, limesema watalaam katika kampuni hiyo wanatarajiwa kumaliza kazi hiyo kwa muda wa miezi minane na baadaye kupisha kuanza ujenzi wa bomba hilo.

Mwaka uliopita, Uganda na Tanzania zilikubaliana kujenga bomba hilo la mafuta kwa gharama ya Dola za Marekani Bilioni 3.55.

Bomba hilo la mafuta linalotarajiwa kuwa na urefu wa Kilomita 1,445, litaisaidia Uganda kuuza mafuta yake katika soko la Kimataifa, yakisafirishwa kutoka bandari ya Tanga.

Kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya Total imekubali kufadhili mradi huo.

Uganda inatarajiwa kuanza kuzalisha na kusafirisha mafuta yake kuanzia mwaka 2020.