KENYA

Mahakama nchini Kenya yatishia kuwafunga jela viongozi wa Madaktari

Mahakama inayoshughulikia utatuzi wa mizozo ya ajira nchini Kenya, imewapa viongozi wa Madaktari muda wa wiki mbili kusitisha mgomo unaoendelea la sivyo, wafungwe jela kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Picha ikionesha manesi na madaktari wakiwa kwenye mgomo wao kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao ya mshahara.
Picha ikionesha manesi na madaktari wakiwa kwenye mgomo wao kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao ya mshahara. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Jaji Hellen Wasilwa ametoa agizo hilo katika Mahakama hiyo jijini Nairobi, na kuwaambia viongozi hao ambao hawakuwepo Mahakamani kupata mwafaka kati yao na serikali kwa muda waliopewa.

Aidha, amewashutumu viongozi hao kama viongozi dhaifu wasioweza kufanya maamuzi kwa niaba ya wanachama wao.

Agizo hili linamaanisha kuwa viongozi hao wamefungwa tayari kifungo cha nje cha mwezi mmoja, na ikiwa hawatakuwa wamesitisha mgomo huo, watafungwa jela kwa muda wa wiki mbili.

Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari nchini humo Ouma Oluga, amesema hawatatishwa na Mahakama wala serikali na watarejea kazini pale tu serikali itakapotekeleza mkataba wa kuwaongezea mshahara kwa asilimia 300.

Madaktari hao wamekataa pendekezo la serikali kuwaongezea mshahara kwa asilimia 40.

Mgomo huu umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kuzorotesha huduma za afya katika hospitali za umma.

Serikali imetishia kuwafuta kazi Madaktari wote wanaogoma.