BURUNDI-EU-AMISOM

Burundi yaanza mchakato wa kuondoa wanajeshi wake Somalia

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza akikagua gwaride la heshima la askari wake walioko nchini Somalia, 22 April 2014.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza akikagua gwaride la heshima la askari wake walioko nchini Somalia, 22 April 2014. UN Photo/Ilyas A Abukar

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amezitaka wizara ya ulinzi na ya mambo ya nje, kuanza mchakato wa kuondoa wanajeshi wake kutoka nchini Somalia. Uamuzi huu unakuja baada ya serikali ya Burundi kutishia mara kadhaa kuwaondoa askari hao nchini Somalia kufuatia mvutano kati yake na Umoja wa Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Makamu wa kwanza wa rais Gaston Sindimwo ameliambia shirika la habri la AFP kwamba serikali ya Burundi imeamua kuondoa wanajeshi wake kufuatia uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kusitisha malipo kwa serikali ya Burundi ya Euro milioni tano kila mwezi kama mshahara wa wanajeshi hao.

Mwezi Novemba mwaka jana, Umoja wa Afrika ulipinga uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kusitisha malipo ya mishahara kwa wanajeshi hao kupitia kwa serikali, ukionya kuwa ingekuwa na madhara kwa kikosi cha Amisom.

Burundi ina askari 5,400 katika kikosi cha Amison, na inachukua nafasi ya pili kwa kuchangia wanajeshi wengi zaidi katika kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom) baada ya Uganda. Amisom inafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya.

Burundi imewekewa vikwazo mbalimbali kufuatia uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu kinyume na katiba ya nchi ya Burundi ambayo inasema wazi kuwa rais anapaswa kuongoza nchi hiyo kwa mihula miwili pekee kama atakua amechaguliwa kwa mara ya pili.

Machafuko nchini Burundi yamesababiha watu zaidi ya 600 kupoteza maisha na maelfu kuyahama makazi yao na kukimbilia nchi jirani.