BURUNDI-MAZUNGUMZO

Wanasiasa wa Burundi waomba kukutana ana kwa ana na serikali

Askari wa Burundi wakipiga doria katika mitaa ya Bujumbura, baada ya shambulio la guruneti, Februari 3, 2016.
Askari wa Burundi wakipiga doria katika mitaa ya Bujumbura, baada ya shambulio la guruneti, Februari 3, 2016. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimama

Wanasiasa wa Burundi wamemuomba msuluhishi wa mzozo wa kisiasa nchini mwao kuwakutanisha moja kwa moja na serikali ili kufikia mwafaka wa kudumu. Wito huu umekuja baada ya mwezeshaji wa kutatua mzozo huu rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa kukutana Jumatatu wiki hii na wanasiasa kutoka pande zote mbili.

Matangazo ya kibiashara

Katika mazunguzo hayo wasiasa hao wameonekana kutofautiana kuhusu maswala nyeti, hususan swala la Muhula wa 3 ambalo upinzani uliougenini unasisitiza kwamba ndio tatizo la mzozo uliopo, huku wale wanaounga mkono utawala wakiona kwamba swala hilo limepitwa na wakati.

Jacques Bigirimana kutoka chama cha FNL kinachotambulika serikalini kinachounga mkono utawala wa rais Pierre Nkurunziza ameomba msuluhishi awakutanishe ana kwa ana ili Warundi wamalize matatizo yao.

 

Upande wake William Munyembabazi kutoka chama cha CNDD cha Leonard Nyangoma aliepo uhamishoni anaona kwamba msuluhishi mwenyewe licha ya kauli yake ya kupinga muhula wa 3 anakiri kuona uwepo wa matatizo makubwa nchini Burundi.

 

Wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa wanaona kuwa mjadala kuhusu muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, ulipaswa kuwepo kwenye ajenda za mratibu wa mazungumzo ya amani ya Burundi, kuliko kupendekezwa kuwekwa kando, kwa kile wanachosema kukwepa mjadala huu kutafanya mazungumzo kuwa magumu zaidi.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa mahakama ya katiba ilitafsiri visivyo suala la muhula wa rais Nkurunziza na kwamba msuluhishi hakutakiwa kuliweka kando suala hili ikiwa kweli anataka suluhu ya kisiasa ipatikane.

Mkutano huo umesusiwa kwa sehemu kubwa na wapinzani kutoka muungano wa CNARED unaendelea kusisitiza swala la muhula wa 3 na kupinga kauli ya msuluhishi, huku wakihoji mualiko wa wanasiasa kutoka Burundi wakati ambapo hapo awali ilidaiwa kwamba ni mkutano wa wanasiasa ambao wanaishi uhamishoni ambao hakukutana nao wakati wa ziara yake nchini Burundi mwishoni mwa mwaka uliopita.