BURUNDI-AU-EU

Serikali ya Burundi yaahirisha mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake Somalia

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza akikagua gwaride la heshima la askari wake walioko nchini Somalia, 22 April 2014.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza akikagua gwaride la heshima la askari wake walioko nchini Somalia, 22 April 2014. UN Photo/Ilyas A Abukar

Serikali ya Burundi imesema kuwa, haitaendelea mbele na mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake walioko Somalia chini ya AMISOM, baada ya kufikia makubaliano kuhusu malipo ya mshahara wao.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Ulaya ndio inaolipa mishahara ya vikosi vya AMISOM, fedha ambazo husambazwa na umoja wa Afrika, lakini utawala wa Bujumbura ulikuwa haujapokea malipo yoyote kwa miezi kadhaa kutokana na wanadiplomasia wa Ulaya kukwepa kulipa fedha hizo moja kwa moja kwa Serikali ya Burundi iliyowekewa vikwazo na umoja huo.

Hata hivyo makamu wa kwanza wa rais wa Burundi, Gaston Sindimwo, amesema hivi sasa wamepata suluhu ambayo inalinda uhuru na maslahi ya taifa lao na kwamba suala la kuwaondoa wanajeshi wake kwenye vikosi vya AMISOM halitakuwepo.

Jumatatu ya wiki hii, makamu wa kwanza wa rais Sindimwo alitangaza kuwa nchi yao imeshaanza kuwaondoa sehemu ya wanajeshi wake 5400 kutoka Somalia, tangazo lililowafanya maofisa wa umoja wa Afrika kufanya ziara ya haraka jijini Bujumbura, wakiongozwa na Smail Chergui.

Kwa mujibu wa makubaliano haya, mshahara wa wanajeshi hao, sasa utapitia kwenye benki kuu ya nchi hiyo na sio kwenye benki binafsi kama ilivyokuwa ikifanyika sasa.

Hata hivyo haijafahamika mara moja, ikiwa umoja wa Ulaya utakubali kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya umoja wa Afrika na Serikali ya Burundi.