RWANDA

Mwanasiasa wa upinzani Thomas Nahimana adai kunyimwa idhini ya kurudi nyumbani

Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda  Thomas Nahimana
Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda Thomas Nahimana therwandan

Mwanasiasa wa upinzani na Padri  wa Kanisa Katoliki nchini Rwanda Thomas Nahimana amedai kunyimwa idhini ya kurudi nyumbani.

Matangazo ya kibiashara

Nahimana alitarajiwa kurejea nchini Rwanda siku ya Jumatatu akitokea jijini Brussels nchini Ubelgiji, lakini hakuweza kufanya hivyo baada ya kudai kuwa serikali ya Kigali inaendelea kumwekea vikwazo.

Mwanasiasa huyo ambaye anatumia pasi ya usafiri ya Ufaransa, tayari ametangaza nia ya kuwania urais nchini humo mwezi Agosti mwaka huu.

Mwezi Novemba mwaka uliopita, alizuiliwa jijini Nairobi nchini Kenya wakati anajiandaa kuabiri ndege kwenda jijini Kigali, baada ya serikali ya Rwanda kuitaka Kenya kutomruhusu kufika Kigali.

Yves Butera, msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini Rwanda amesema kuwa Padri huyo atakaribishwa nchini Rwanda kama raia mwingine.

Hata hivyo, amemshtumu kwa kutoifahamisha idara ya Uhamiaji ya Rwanda kuwa amekuwa raia wa Ufaransa wakati huu akiendelea kutumia pasi ya Rwanda iliyopitwa na wakati.

Nahimana amekuwa akihusishwa na mauaji ya kimbari mwaka 1994 kutokana na matamshi ambao amekuwa akiyatoa akiwa nje ya nchi.

Mwaka 20O5, alitoroka nchini Rwanda na kuachana na majukumu yake ya kuongoza Kanisa Katoliki katika jimbo la Cyangugu Kusini Magharibi mwa Rwanda.