SUDAN KUSINI

Umoja wa Mataifa wasisitiza umuhimu wa jeshi la Ukanda kutumwa Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasema kuna umuhimu mkubwa sana wa kutumwa kwa jeshi la ukanda wa Afrika Mashariki nchini Sudan Kusini.

Askari wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, wakipiga doria kwenye kambi yao, Julai 20, 2016.
Askari wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, wakipiga doria kwenye kambi yao, Julai 20, 2016. REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Baraza hilo kwa mwezi wa Januari Olof Skoog, amesema jeshi hilo linahitajika nchini humo haraka iwezekanavyo ili kusaidiana na lile la Umoja wa Mataifa
kutuliza mapigano yanayoendelea lakini pia kutatua hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.

Baraza hilo limesema linasikitishwa sana na mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo huku maelfu ya raia wa nchi hiyo wakikosa mahitaji muhimu kama chakula, dawa na makaazi baada ya kukimbia vita.

Miezi sita iliyopita, Baraza hilo la UN lilikubali kutumwa kwa kikosi hicho cha wanajeshi 4,000 jiji Juba lakini serikali ya rais Salva Kiir imekuwa ikikataa kuliruhusu kuja kwa jeshi hilo kwa madai kuwa nchi hiyo sasa ina amani.

Rwanda na Ethiopia zinasema ziko tayari kutuma wanajeshi wao katika kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa.

Kenya ambayo iliwaondoa wanajeshi wake mwaka uliopita nchini humo, imeiambia Umoja wa Mataifa kuwa inaweza kushiriki katika Operesheni hiyo ikiwa kutakuwa na mazungumzo kati yake na wakuu wa Umoja huo.