KENYA-SIASA

Upinzani nchini Kenya wadai serikali inatumia Shirika la Ujasusi NIS kuwasajili wageni kama wapiga kura

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Cord Raila Odinga, anaishtumu serikali kwa kutumia idara ya ujasusi nchini humo NIS kuwasajili raia wa nchi jirani kama wapiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga REUTERS/Noor Khamis
Matangazo ya kibiashara

Odinga amesema kuwa Shirika hilo limeweka mikakati ya raia wanaoishi katika mpaka na Kenya ambao ni raia wa Uganda na Ethiopia kuja nchini kujiandikisha.

Aidha, amedai kuwa serikali inapanga kutumia mbinu iliyotumia mwaka 2007 na 2013 ili kuiba kura, suala ambalo amesema upinzani hautakubali.

“Lazima idara hii ijitokeze na kuacha inachokifanya, hatutakubali kinachoendelea,” alisema Odinga.

“Inabidi Tume ya Uchaguzi iachiwe kazi ya kuwasajili wapiga kura,” aliongeza Odinga.

Hivi karibuni Odinga na kinara mwenzake wa upinzani Kalonzo Musyoka, walidai kuwa namba za vitambulisho vyao vimetumiwa kuwasajili wapiga kura wengine, madai yaliyoshughulikiwa na Tume ya Uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya IEBC wiki iliyopita, ilianza zoezi la mwezi mmoja kuwasajili wapiga kura wapya.

IEBC imesema zoezi hilo ambalo linatarajiwa kumalizika Februari tarehe 14, linawalenga wapiga kura wapya Milioni 6 ambao hawakupiga kura mwaka 2013.

Wapinga kura Milioni 24 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi la kupiga kura tarehe 8 mwezi Agosti mwaka huu baada ya zoezi hili kukamilika.

Rais Uhuru Kenyatta anatetea wadhifa huo. Muungano wa upinzani bado haujatangaza mgombea wake.