Mahakama yawapa viongozi wa Madaktari nchini Kenya siku tano kusitisha mgomo unaoendelea
Mahakama inayoshughulikia mizozo ya ajira nchini Kenya, imewapa viongozi wa Chama cha Madaktari nchini humo siku tano kusitisha mgomo unaoendelea, la sivyo watafungwa jela mwezi mmoja.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Jaji Hellen Wasilwa amewataka pia Madaktari hao kuendelea kuzungumza na serikali ili kufikia mwafaka kwa muda huo waliopewa.
Viongozi wa Madaktari hao ni pamoja na Mwenyekiti wao Samuel Oroko Oregi, Titus Ondoro, Allan Ochanji, Fredrick Ouma Oluga, Hamisi Mwachonda Chibanzi, Daisy Korir na Evelyne Chege.
Madaktari nchini humo kwa siku ya 53 leo wanaendelea na mgomo wakitaka kutekelezwa ipasavyo makubaliano waliyofikia mwaka 2013.
Serikali imesema iko tayari kuwapa nyongeza ya mshahara kwa asilimia 40, nyongeza ambayo Madaktari wamekataa na kusisitiza kuwa wanataka nyongeza ya asilimia 300.
Mbali na suala la mshahara, Madaktari hao wanataka kuboreshwa kwa mazingira ya kufanya kazi, kuajiriwa kwa Madaktari zaidi lakini pia kuwepo kwa mikakati ya kuwapa mafunzo ya mara kwa mara kuimarisha taalum yao.
Mbali na madai hayo, Madaktari hao wanataka kulipwa wanapofanya kazi ya ziada lakini pia kufanya kazi kwa saa nane kwa siku.