UGANDA

Rais Museveni aadhimisha miaka 31 madarakani

Rais wa Uganda Yoweri Museveni anaadhimisha miaka 31 ya kuongoza nchi hiyo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni RFI
Matangazo ya kibiashara

Siku kama ya leo mwaka 1986, vikosi vya NRA vikiongozwa na Museveni baada ya vita vya miaka mitano msituni, vilifanikiwa kufika jijini Kampala na kuondoa utawala wa Milton Obote.

Museveni mwenye umri wa miaka 72, amekuwa akisema kuwa tangu alipoingia madarakani amesaidia pakubwa sana kuimarisha maisha ya raia wa nchi hiyo.

Kauli mbinu ya uongozi wa rais Museveni ya kukaa madarakani kwa miaka 31 ni mafanikio ya chama tawala NRM, katika nyanja mbalimbali nchini humo.

Mambo mawili muhimu ambayo rais Museveni amesifiwa kufanikisha katika uongozi wake wa miaka 31 ni kuimarisha hali ya usalama, utulivu na amani nchini humo na kufanikisha kuwaondoa waasi wa ADF Nalu na LRA.

Aidha, uongozi wake umesaidia sana kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Wakati akiingia madarakani maambukizi yalikuwa katika asilimia 15 na sasa yamepungua na kufikia asilimia 6 hivi baada ya serikali kuzindua mipango mbalimbali ya kupambana na janga hili.

Mbali na mafanikio hayo, kiongozi huyo amekuwa akikosolewa kwa kushindwa kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na raia wengi kuendelea kuishi kwa umasikini.

Aidha, anaendelea kushtumiwa kwa kukaa madarakani kwa muda mrefu baada ya kuondoa mihula ya uongozi wa urais.

Museveni ni miongoni mwa viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika ambao wameendelea kukaa madarakani kwa muda mrefu.

Viongozi hao ni pamoja na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, wa Equatorial Guinea, Jose Eduardo dos Santos wa Angola, Robert Mugabe wa Zimbabwe na Paul Biya wa Cameroon.