Tanzania kupewa Dola Milioni 305 na Benki ya Dunia
Imechapishwa:
Tanzania itapokea mkopo wa Dola Milioni 305 kutoka kwa Benki ya dunia ili kupanua bandari ya Dar es salaam. Hatua hii imekuja wakati huu bandari hiyo inahudumia mataifa jirani kama Zambia, Rwanda, Malawi, na Burundi imekuwa ikishuhudia msongamano mkubwa.
Waziri wa Fedha nchini humo Philip Mpango amesema Benki ya dunia imekubali kutoa mkopo huo.
Mwezi Oktoba Tanzania ilitajwa na Benki ya Dunia kuwa miongoni mwa mataifa machache duniani ambayo yamefanikiwa pakubwa kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini.
Kwenye ripoti ya benki hiyo kuhusu usawa duniani, Tanzania imeorodheshwa pamoja na Cambodia na Brazil kama nchi tatu zilizopiga hatua sana.
Nchini Tanzania, ripoti hiyo inasema, ufanisi ulipatikana katika kipindi ambacho taifa hilo lilipata ukuaji thabiti wa uchumi wa kiwango cha wastani cha asilimia 6.5 kila mwaka kati ya 2004-2014.
"Kiwango cha umaskini kitaifa kilishuka kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012," ripoti ya benki hiyo inasema.