KENYA-SOMALIA

Al Shabab yavamia kambi ya wanajeshi wa Kenya katika eneo la Kulbiyow

Kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia, limeshambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya katika eneo la Kulbiyow karibu na mpaka na nchi hiyo.

Wanajeshi wa AMISOM nchini Somalia
Wanajeshi wa AMISOM nchini Somalia AFP/AU-UN/Stuart Price
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa kundi la Al Shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab amesema washambuliaji wake wamefanikiwa kuwauawa wanajeshi 57 wa Kenya waliokuwa katika kambi hiyo baada ya kuwashambulia Ijumaa alfajiri.

Hata hivyo, jeshi la Kenya kupitia msemaji wake Luteni Kanali Paul Njuguna, amekanusha madai ya wanajeshi wa KDF kuuawa na kusema kilichotokea ni tishio la shambulizi ambalo halikufanikiwa.

Aidha, ameeleza kuwa jeshi la Kenya linapambana na wanamgambo hao na kuongezea kuwa wengi wao wametoroka.

Mwaka uliopita, mwezi Januari kundi la Al Shabab walivamia kambi nyingine ya KDF katika eneo la El Adde, na kusababisha vifo vya wanajeshi 100.

Jeshi la Kenya linashirikiana na wanajeshi wengine kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika chini ya mwavuli wa AMISOM kupambana na kundi la Al Shabab ambalo linataka kuiangusha serikali ya Mogadishu inayoungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.