KENYA

Viongozi wa chama cha Madaktari nchini Kenya wafungwa jela mwezi mmoja

Viongozi wa chama cha Madaktari nchini Kenya wamefungwa jela mwezi mmoja baada ya kukaidi agizo la Mahakama inayoshughulikia maswala ya ajira kusitisha mgomo unaoendelea kwa zaidi ya siku 70 sasa.

Picha ikionesha manesi na madaktari wakiwa kwenye mgomo wao kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao ya mshahara.
Picha ikionesha manesi na madaktari wakiwa kwenye mgomo wao kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao ya mshahara. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Jaji Hellen Wasilwa akitoa uamuzi huo jijini Nairobi, amesema amelazimika kutoa kifungo hicho, baada ya viongozi hao kushindwa kutii Mahakama lakini pia kushindwa kuafikiana na serikali kuhusu madai yao.

Aidha, Jaji huyo amesema viongozi hao saba wa Madaktari wameshindwa kuithibitisha Mahakama ni kwanini wasifungwe jela kwa kukaidi agizo hilo.

Ombi la Mawakili wa Madaktari hao halikukubaliwa na Mahakama baada ya kifungo hicho kuahirishwa mara tatu, ili kutoa nafasi ya mazungumzo.

Madaktari nchini humo wamekataa nyongeza ya asilimia 40 iliyotolewa ili warudi kazini na badala yake wameendelea kusisitiza nyongeza ya asilimia 300 kama walivyokubaliana na serikali mwaka 2013.

Mbali na nyongeza na mshahara, Madaktari wanataka kuboreshewa mazingira ya kazi, kupewa mafunzo zaidi pamoja na kununuliwa kwa vifaa vipya na kwa kisasa.

Mgomo huu umesitisha huduma katika hospitali za umma nchini humo.