KENYA-AFYA-MAANDAMANO

Kenya yaombwa kutafutia uvumbuzi madai ya madaktari

Polisi wa kuzima ghasia akitoa ulinzi mbele ya maandamano ya madaktari wa Kenya mjini Nairobi, Februari 13, 2017.
Polisi wa kuzima ghasia akitoa ulinzi mbele ya maandamano ya madaktari wa Kenya mjini Nairobi, Februari 13, 2017. REUTERS/Thomas Mukoya

Wanaharakati nchini Kenya, wameitaka serikali kupitia wizara ya Afya kuhakikisha viongozi wa madaktari waliohukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela kwa kudharau amri ya mahakama wanaachiwa huru ili kutoa nafasi ya mazungumzo zaidi kupata muafaka wa mgomo unaoendelea.

Matangazo ya kibiashara

Akihojiwa na kamati ya bunge la Seneti Jumanne wiki hii, waziri wa Afya, Cliopa Mailu, ametoa wito wa madaktari hao kuachiwa huru ili kuruhusu mazungumzo kuendelea.

Mgomo wa madaktari nchini Kenya umechukua sura nyingine, baada ya Jumanne wiki hii chama cha madaktari pwani ya nchi hiyo mjini Mombasa, kutangaza mgomo wa saa 48 kwa hospitali za kibinafsi, kupinga hatua ya wenzao kuswekwa jela kutokana na kukaidi amri ya mahakama.

Bila shaka mgomo huu utaathiri pakubwa wagonjwa ambao wengi walikimbilia hospitali za kibinafsi baada ya zile za serikali madaktari wake kugoma.

Viongozi wa chama cha Madaktari nchini Kenya walifungwa jela mwezi mmoja baada ya kukaidi agizo la Mahakama inayoshughulikia maswala ya ajira kusitisha mgomo unaoendelea kwa zaidi ya siku 70 sasa.

Jaji Hellen Wasilwa akitoa uamuzi huo jijini Nairobi, alisema amelazimika kutoa kifungo hicho, baada ya viongozi hao kushindwa kutii Mahakama lakini pia kushindwa kuafikiana na serikali kuhusu madai yao.

Aidha, Jaji huyo alisema viongozi hao saba wa Madaktari wameshindwa kuithibitisha Mahakama ni kwanini wasifungwe jela kwa kukaidi agizo hilo.

Ombi la Mawakili wa Madaktari hao halikukubaliwa na Mahakama baada ya kifungo hicho kuahirishwa mara tatu, ili kutoa nafasi ya mazungumzo.

Madaktari nchini humo wamekataa nyongeza ya asilimia 40 iliyotolewa ili warudi kazini na badala yake wameendelea kusisitiza nyongeza ya asilimia 300 kama walivyokubaliana na serikali mwaka 2013.

Mbali na nyongeza na mshahara, Madaktari wanataka kuboreshewa mazingira ya kazi, kupewa mafunzo zaidi pamoja na kununuliwa kwa vifaa vipya na kwa kisasa.

Mgomo huu umesitisha huduma katika hospitali za umma nchini humo.