BURUNDI-EAC-USALAMA

Afisa wa zamani wa EAC kutoka Burundi azuiliwa Dar es Salaam

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania wanamzuiwa Callixte Nsengiyumva, mfanyakazi wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Burundi.

Askari wa Burundi wakipiga doria katika mitaa ya Bujumbura, baada ya shambulio la guruneti, Februari 3, 2016.
Askari wa Burundi wakipiga doria katika mitaa ya Bujumbura, baada ya shambulio la guruneti, Februari 3, 2016. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimama
Matangazo ya kibiashara

Afisaa huyo wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupinga muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza, aliomba hifadhi ya ukimbizi nchini Tanzania, baada ya mkataba wake na Jumuiya hiyo kumalizika.

Alikamatwa Jumatatu asubuhi na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania wakati ambapo alikua akitafuta jibu kuhusu ombi lake, kwa mujibu wa mmoja wa familia yake ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Callixte Nsengiyumva anazuiliwa Kiliwa Road Police, mjini Dar es Salaam, huku akitishiwa kusafirishwa nchini Burundi.

Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu nchini Burundi na yale ya ukanda wa Maziwa Makuu yanaomba serikali ya Tanzania hasa Rais John Pombe Magufuli na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi kuingilia kati ili kumlindia usalama afisa huyo wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mashirika hayo ya haki za binadamu yana hofu kwamba Callixte Nsengiyumva anaweza kumaliziwa maisha iwapo atasafirishwa nchini Burundi, kwani ni miongoni mwa watu waliompinga kwa mara ya kwanza Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu, akisema kuwa ni kinyume na mkataba wa amani wa Arusha pamoja na katiba ya nchi ambayo ni sheria mama.

Mashirika ya haki za binadamu yanabaini kwamba kama Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) itabaki jumuiya ya wananchi wa mataifa matano wanachama wa EAC kuliko kuwa kundi la viongozi wa nchi hizo, Jumuiya hiyo ina wajibu wa kumlindiia usalama Callixte Nsengiyumva na kumlindia haki zake za msingi.

Serikali ya Tanzania haijanzungumza kuhusu kukamatwa kwa afisa huyo wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.