BURUNDI-EU-USHIRIKIANO

Burundi: Bunge laomba msaada kutoka umoja wa Ulaya

Katika taarifa ya pamoja iliyosainiwa na Spika wa Bunge na rais wa Baraza la Seneti vya Burundi, wawili hao wamethibitisha kwamba karibu sekta zote zinakabiliwa na hali ya sintofahamu kutokana na ukosefu wa misaada kutoka nje.

Spika wa Bunge la Burundi, Pascal Nyabenda.
Spika wa Bunge la Burundi, Pascal Nyabenda. AFP PHOTO / LANDRY NSHIMIYE
Matangazo ya kibiashara

Taarifa hii iliyotolewa Jumatatu hii, Februari 27, 2017 ambayo ilisomwa na Makamu wa pili wa Spika wa Bunge Chantal jocky Nkurunziza baada ya tangazo la Bunge la Canada. Hivi karibuni Bunge la Canada lilielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kutisha ya kibinadamu inayoendelea kushuhudiwa nchini Burundi.

Taasisi hizo mbili za Burundi zimetolea wito Umoja wa Ulaya kutoa misaada yake kwa wananchi wa Burundi waishio mikoani kama unavyofanya kwa wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchi jirani.

Licha ya njaa inayoelezwa nchini Burundi, serikali ya Bujumbura imekua ikiendelea kuandaa maandamano dhidi ya Umoja wa Ulaya (EU) kila Jumamosi. Viongozi wa ngazi ya juu serikalini ambao hushiriki maandamano hayo wanatoa hotuba zao kila mara kwamba Burundi ni nchi huru na haihitaji msaada kutoka Umoja wa Ulaya.