KENYA-MOMBASA

Mombasa: Marekani, Denmark na Serikali ya Kenya zimezindua kampeni kupambana na itikadi kali

Wapiganaji wa Al-Shabab na wale wa Hizbul wakiwa mjini Mogadishu, 2009.
Wapiganaji wa Al-Shabab na wale wa Hizbul wakiwa mjini Mogadishu, 2009. (Photo : AFP)

Mabalozi wa Marekani na Denmark nchini Kenya pamoja maafisa wa usalama, wamezuru kaunti ya Kwale kusini mwa pwani ya Kenya kuzindua mpango maalum, wa kukabiliana na tatizo la itikadi kali ya kidini ikiwa ni katika harakati za kukabilina na ugaidi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec ameipongeza Serikali na wadau, kutokana na juhudi zao za kukabiliana na itikadi kali za dini, ambapo amesema dhuluma za kihistoria na unyanyasaji katika jamii vinafaa kutatuliwa kwa kuwa huenda vinachangia vijana kujiunga na makundi ya kigaidi.

Jimbo la Kwale ni miongoni mwa maeneo yalioyoathirika na tatizo hilo, baada ya vijana wengi kurejea nchini humo baada ya kujiunga na kundi la kigaidi la Alshabab.

Kwa upande wake balizi wa Denmark nchini Kenya, Mette Knudsen, amesema kuna umuhimu wa asasi za kiraia na taasisi za Serikali kufanya kazi kwa pamoja ili kuelezana na kutambua chanzo hasa cha tatizo hilo.

Katika hatua nyingine, kamishna wa tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa nchini humo, NCIC, Iren Wanyoike ametoa changamoto kwa serikali kuhusisha wanawake majumbani akisema wanataarifa muhimu za kiusalama ambazo zitasaidia kukabili itikadi kali.