UGANDA-ICGLR-M23-USALAMA

ICGLR kutathimini mbinu ya kutokomeza M23 na ADF

wapiganaji wa kundi la zamani la M23, Februari 2014.
wapiganaji wa kundi la zamani la M23, Februari 2014. AFP PHOTO/ ISAAC KASAMANI

Kamati ya pamoja inayoratibu maswala ya Usalama katika Jumuia ya nchi za maziwa makuu imeanza kufanya kazi Wilayani Kasese nchini Uganda.

Matangazo ya kibiashara

Kamati hiyo itasaidia kukusanya taarifa muhimu kufanikisha vita dhidi ya waasi Mashariki mwa DRC.

Watalaam kutoka Uganda, Kenya, Tanzania na DRC wanakusanya taarifa za Kiinteljensia zinazoweza kuwasaidia kupambana na makundi ya waasi Mashariki mwa DRC, kuhakikisha kuwa eneo la Maziwa Makuu linakuwa salama.

Mwanzoni mwa wiki hii ujumbe wa maafisa wa Jumuia ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulipelekwa nchini Uganda kuchunguza ikiwa kweli waasi wa zamani wa kundi la M23 wametoroka katika kambi waliyokuwa wamehifadhiwa.

Ujumbe huo ulitembelea maeneo mengi ikiwemo Kishobo, Bihanga, Nakivale upande wa Uganda.

Hivi karibuni Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC lilipambana na kundi la waasi walioripotiwa kutoka Uganda, katika milima ya Songa wilayani Rutshuru mashariki mwa DRC.

Hata hivyo Rwanda iliwahi kutangaza kwamba iliwakamata wapiganaji wa kundi la zamani la waasi la M23, ambao waliingia nchini humo baada ya kukimbia mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kundi la la waasi la Uganda la ADF linaloendelea na harakati zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekua likihatarisha usalama wa raia katika maeneo ya Beni na Butembo. Watu kadhaa wameua na kundi hilo na kusababisha wakaazi wa vitongoji vya mji wa Beni kuyahama makaazi yao.