KENYA

Kenya: Serikali yaagiza madaktari kurejea kazini haraka, wenyewe wagoma

Madaktari nchini Kenya wakiwa na mabango kushinikiza kusikilizwa wakati walipoandamana hivi karibuni jijini Nairobi.
Madaktari nchini Kenya wakiwa na mabango kushinikiza kusikilizwa wakati walipoandamana hivi karibuni jijini Nairobi. REUTERS/Thomas Mukoya

Madaktari nchini Kenya wamesema hawatarejea kazini licha ya agizo la Serikali kuwataka kurejea kazini haraka iwezekanavyo na kutangaza pia kuondoa nyongeza ya asilimia 50 waliyokubali kuilipa hapo awali.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili la kushangaza la Serikali limetolewa baada ya mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kugonga mwamba, madaktari hao wanataka nyongeza ya asilimia 150 hadi 180.

Kwenye makubaliano mapya yaliyofikiwa kwa msaada wa wapatanishi uliojumuisha ujumbe wa viongozi wa dini, madaktari hao walitakiwa kutia saini hati ya kukubali kurejea kazini na kuanza kazi mara moja, lakini hata hivyo viongozi wa madaktari wamegoma kutia saini.

Mgomo huu unaojumuisha zaidi ya madaktari elfu 5 nchini Kenya kutoka kwenye hospitali za uma, sasa umefikia miezi mitatu na kwa hali hii hakuna dalili ya kusitishwa kwa mgomo wenyewe.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta anasema kuwa madaktari hao wanailaghai na kuihujumu Serikali yake.

Mgomo huu ambao ulianza mwezi Desemba mwaka jana, umeibusha hasira miongoni mwa wa Kenya na kuongeza shinikizo kwa Serikali ya rais Kenyatta kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka huu.

Makubaliano ya awali na haya yaliyokuwa yanaratibiwa na viongozi wa dini, yalitaka pia kuboreshwa kwa mazingira ya kazi ya madaktari, kurekebishwa kwa mifumo ya kazi na vigezo vitakavyotumika kupandishwa vyeo.

Mgomo huu pia umesababisha hata baada ya viongozi wa madaktari nchini humo kutupwa jela baada ya kukutwa na hatia ya kukaidi amri ya mahakama kusitisha mgomo.