SUDAN KUSINI-JAPAN

Japan kuondoa wanajeshi wake Juba rais Kiir aitisha mazungumzo ya kitaifa

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir akizungumza wakati wa kumbukumbu ya marehemu John Garang jijini Juba, Machi 10, 2017
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir akizungumza wakati wa kumbukumbu ya marehemu John Garang jijini Juba, Machi 10, 2017 REUTERS/Jok Solomon

Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, ametangaza mpango wa nchi yake kuanza kuwaondoa wanajeshi wake wanaohusika na ujenzi kwenye taifa la Sudan Kusini ifikapo mwezi Mei mwaka huu, uamuzi unaokuja ikiwa ni miaka mitano ya uwepo wa vikosi vyake Sudan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Waziri mkuu Abe, amewaambia waandishi wa habari kuwa amefanya tathmini ya namna ambavyo wanajeshi wake wa ujenzi wa miundo mbinu wamefanya kazi mjini Juba, na kwamba ameridhishwa na hatua iliyopigwa na inafikia ukingoni.

Katibu mkuu wa ziara ya ulinzi ya Japan, Yoshihinde Suga, amesisitiza kwenye mkutano tofauti na waandishi wa habari kuwa kuondoka kwao nchini Sudan Kusini hakuna uhusiano wowote na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo.

Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe.
Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe. REUTERS/Issei Kato

Kwa sasa nchi ya Japan ina wanajeshi wanaojihusisha na masuala ya ujenzi wapatao 350 ambao wako kwenye sehemu ya vikosi vya umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini Sudan Kusini wakiwa na jukumu la ujenzi wa barabara na kuzifanyia ukarabati.

Katika hatua nyingine, rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir ametangaza kuwa mwishoni mwa juma hili, nchi hiyo itafanya mkutano wa kitaifa wa maridhiano, mazungumzo yanayolenga kuzungumzia shida zinazoikabili nchi hiyo na kupata muafaka.

Hata hivyo mazungumzo hayo yamekashifiwa vikali na viongozi wa makundi ya waasi nchini humo ambao wanasema mazungumzo hayo hayana tija kwakuwa hata watakaohusika sio wahusika wakuu wa yanayoshuhudiwa nchini Sudan Kusini.

Mwanzoni mwa mwaka huu rais Kiir alisema kuwa kuna haja ya kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa ili kusaka suluhu ya pamoja na kuwaunganisha wananchi ambao wameendelea kugawanyika kwa misingi ya ukabila.

Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani, imejikuta ikitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe toka mwaka 2013, baada ya rais Kiir kumfuta kazi aliyekuwa makamu wake wa rais Riek Machar ambaye anaongoza uasi kuipinga Serikali ya Juba.