UGANDA

HRW: Watu 155 waliuawa kwenye makazi ya mfalme wa Rwenzururu nchini Uganda

Silaha zilizokamatwa wakati wa operesheni ya kumkamata mfalme wa Rwenzururu, nchini Uganda, Charles Wesley Mumbere
Silaha zilizokamatwa wakati wa operesheni ya kumkamata mfalme wa Rwenzururu, nchini Uganda, Charles Wesley Mumbere REUTERS/James Akena

Watu zaidi ya 155, wakiwemo watoto 15, waliuawa wakati wa makabiliano kati ya vikosi vya Uganda na walinzi wa mfalme wa Rwenzururu magharibi mwa nchi hiyo mwezi Novemba mwaka jana, imesema ripoti ya Human Rights Watch.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti hii, imekuja baada ya uchunguzi uliofanyika mwezi Januari na Februari na wafanyakazi wa mashirika ya haki za binadamu ambayo yaliwahoji watu zaidi ya 95 ambao ni ndugu ya waliouawa, viongozi wa dini, maofisa usalama na watawala wa Serikali za mitaa, ripoti ambayo inataja idadi zaidi ya ile iliyotangazwa na Serikali ya watu 87.

Novemba 26 na 27 mwaka uliopita wilayani Kasese magharibi mwa Uganda, polisi wa nchi hiyo na jeshi waliungana kutekeleza operesheni ya kuvamia na kushambulia makazi ya mfalme wa Rwenzururu, Charles Wesley Mumbere, huku walinzi wake wakijilinda na silaha za jadi peke yake, imesema ripoti ya Human Rights Watch.

Mamlaka nchini Uganda zenyewe zimetetea operesheni iliyoifanya ambapo inasema walinzi hao walikuwa ni kikundi cha wapiganaji kilichokuwa kimeunda vuguvugu la kuundwa kwa utawala wa Jamhuri ya Yiira kwenye mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Polisi nchini Uganda pia imesema askari wake walishambuliwa kwa mapanga na walinzi wa mfalme huyo.

Hata hivyobaada ya kukamilika kwa operesheni yenyewe, mfalme Charles alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi na uhaini, lakini aliachiwa mwezi Februari.

Shirika la Human Rights Watch linasema ripoti yake ni ripoti huru iliyojumuisha wachunguzi wa kimataifa.

"Shambulizi kwenye ufalme wa Kasese, ambalo lilisababisha vifo vya watu wengi zaidi kuwahi kushuhudiwa kaskazini mwa Uganda kwa zaidi ya miaka 10, ukweli wake haupaswi kufichwa chini ya kapeti" amesema Maria Burnett, kaimu mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Afrika.