TANZANIA-KENYA

Nchi ya Tanzania kutoa madaktari 500 kuisaidia Kenya

Nchi ya Tanzania imekubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaoisaidia nchi hiyo kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo. 

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na mgeni wake Rais wa Tanzania, John Magufuli (kulia), 30 October 2016
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na mgeni wake Rais wa Tanzania, John Magufuli (kulia), 30 October 2016 Kenya State House/ Media handouts
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amekubali kutoa madaktari hao, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya kutoka Kenya uliotumwa na Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta.

Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Waziri wa Afya wa Kenya Dkt. Cleopa Mailu amemueleza Rais Magufuli kuwa, baada ya kutokea mgomo wa madaktari pamoja na uamuzi wa nchi hiyo kugatua madaraka katika sekta ya afya, imebainika kuwa nchi hiyo ina upungufu mkubwa wa madaktari ambao hauwezi kumalizwa kwa kutegemea madaktari wanaosomeshwa nchini humo na badala yake wanahitaji madaktari kutoka nje ya nchi.

Waziri Mailu aliyeongozana na Gavana wa Kisumu Jack Ranguma amesema Kenya ipo tayari kuwalipa stahili zote madaktari 500 watakaopewa na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na mishahara na nyumba za kuishi.

Kwa upande wake waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema Wizara yake ipo tayari kutoa madaktari hao haraka iwezekanavyo kwa kuwa Tanzania inao madaktari wengi wazuri ambao wamemaliza masomo na hawajapata ajira na wengine wamemaliza mikataba yao ya kazi na bado wana uwezo wa kufanya kazi.

“Kwa hiyo nitoe wito kwa madaktari wote Tanzania ambao hawapo katika utumishi wa umma, hawapo katika hospitali teule na ambao hawapo katika hospitali za mashirika yasiyo ya kiserikali wanaolipwa na Serikali, waombe nafasi hizi". alisema waziri Mwalimu

Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii nchini Tanzania, Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii nchini Tanzania, Ummy Mwalimu. YouTube/Screenshot

Waziri Mwalimu ameongeza "Vigezo vikubwa ambavyo tutaviangalia ni kwanza awe amemaliza mafunzo ya vitendo (Internship) na pili awe amesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika, kwa hiyo leo hii tutatoa tangazo na tumefurahi sana kwa sababu tunao madaktari wa kutosha ndani ya nchi na tunaweza kuwapeleka Kenya”.

Mahojiano na Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu Kuhusu Tanzania kutoa Madaktari 500 kwa Kenya

Kwa upande wake Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema, Tanzania imekubali ombi hilo kwa kuwa Kenya ni ndugu, jirani na rafiki wa kweli wa Tanzania na amemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa Tanzania, Ummy Mwalimu, kuharakisha mchakato wa kuwapata madaktari hao ili wawahi kwenda Kenya kutekeleza jukumu hilo.

“Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania, tutawapatia madaktari hao 500 ili wakatoe huduma ya matibabu kwa ndugu zetu waliopo Kenya, na kwa kuwa mmenihakikishia kuwa madaktari wangu mtawalipa mishahara inavyotakiwa, mtawapa nyumba za kuishi, na mtahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri na salama mimi sina tatizo na naamini mambo yatakwenda vizuri” alisema Rais Magufuli.

Ombi hili la Kenya limekuja ikiwa ni juma moja sasa limepita toka madaktari nchini humo wakubaliane na Serikali kusitisha mgomo na kurejea kazini, baada ya kuwa wamegoma kwa zaidi ya miezi mitatu, wakishinikiza nyongeza ya mshahara ya asilimia 300, kulipwa marupurupu yao na kuboreshewa mazingira ya kazi.