Papa aomba msamaha kwa niaba ya kanisa Katoliki nchini Rwanda
Imechapishwa:
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameomba msamaha kwa Kanisa kushindwa kuzuia mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 lakini pia kwa viongozi wa Kanisa hilo ambao huenda walihusika.
Papa Francis ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na rais Paul Kagame katika makao makuu ya Kanisa hilo mjini Vatican.
Kiongozi huyo amesema kuwa amemwomba Mungu kuwasamehe tena viongozi wa Kanisa hilo na watu kutoka jamii ya Wakiristo wengine walioshindwa kuwajibika na kuzuia mauaji hayo ya zaidi ya watu Laki Nane.
Serikali ya Rwanda mwezi uliopita, iliitaka Kanisa Katoliki kuomba radhi kutokana na kuhusika kwao katika mauji hayo mabaya katika historia ya Rwanda.
Viongozi kadhaa wa Kanisa hilo nchini Rwanda wamefunguliwa mashtaka kwa kuhisika na mauaji hayo huku wengine wakifungwa jela na wengine kuachiliwa huru.
Mmoja mwa viongozi wa Kanisa hilo nchini Rwanda ambaye aliwahi kufunguliwa mashtaka ni Marehemu Askofu Augustin Misago, ambaye baadaye aliachiliwa huru mwaka 2000.
Mwezi Novemba mwaka jana, Kanisa Katoliki liliomba radhi kwa kuhusika katika mauaji hayo.