Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi nchini Uganda kuzikwa Jumanne
Imechapishwa:
Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi na msemaji wa jeshi hilo nchini Uganda Felix Andrew Kaweesi anazikwa siku ya Jumanne wilayani Lwengo eneo la Kati ya nchi hiyo.
Kaweesi alipigwa risasi akiwa na dereva wake na mlinzi wake karibu na nyumbani kwake jijini Kampala Ijumaa iliyopita wakati akienda kazini.
Hadi sasa, haijafahamika ni akina nani waliotekeleza kifo hicho na kwanini.
Hata hivyo, uchunguzi wa awali umeonesha kuwa Kaweesi alipigwa risasi na watu waliokuwa kwenye pikipiki mbili na baada ya hatua hiyo, walitoweka.
Mauaji hayo yaliwashangaza raia wa Uganda kwa namna yalivyotekelezwa dhidi ya msemaji huyo wa Polisi ambaye amesifiwa kuwa mtu aliyefanya kazi yake kwa weledi mkubwa.
Rais Yoweri Museveni ameamuru kuwekwa kwa kamera za siri baada ya tukio hilo, kusaidia kuimarisha hali ya usalama jijini Kampala na miji mingine nchini humo.
“Naagiza Wizara ya fedha, ihakikishe kuwa kamera hizo zinawekwa mara moja. Tumekuwa tukiahirisha zoezi hili mara kwa mara lakini sasa ni lazima, lifanyike,” alisema rais Museveni.
Inspekta Mkuu wa Polisi Kale Kaihura, amelaani mauaji ya naibu wake na kusema kuwa waliohusika watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali.
Mauaji haya pia yamelaaniwa pia na wanasiasa nchini humo, akiwemo kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Kizza Besigye ambaye ametaka uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu mauaji haya.
Haya ndio mauaji mabaya dhidi ya afisa mkuu wa serikali kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni, baada ya mauaji mengine kama hayo dhidi ya Joan Kagezi aliyekuwa Kiongozi wa Mashitaka ya umma mwaka 2015.