TANZANIA

Wanahabari nchini Tanzania kutoripoti taarifa kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda Wikipedia

Jukwaa la wahariri nchini Tanzania limewataka wanahabari nchini humo kutoandika, kutangaza au kuripoti habari zozote kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda.

Matangazo ya kibiashara

Wahariri nchini humo wamechukua hatua hiyo baada ya Mkuu huyo wa mkoa kudaiwa kuvamia kituo cha Clouds jijini Dar es salaam akiwa na polisi wenye silaha na kutoa amri ya kutangazwa kwa habari dhidi ya mchungaji maarufu nchini humo Josephat Gwajima.

Katibu wa jukwaa la wahariri nchini humo Nevile Meena, amesema uamuzi wao utaendelea kuwepo hadi pale maamuzi mengine yatakapopatikana.

Meena amekitaja kilichotokea kuingilia uhuru wa vyombo vya Habari na kumtaja Makonda kama adui wa vyombo vya Habari nchini humo.

Wakati hayo yakijiri, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo nchini humo Nape Moses Nnauye amepokea taarifa ya kina kuhusu tukio hilo na kusema kuwa ataiwasilisha ripoti hiyo kwa wakuu wake wa kazi.

Mwenyekiti wa Tume iliyokuwa inachunguza suala hil Deodatus Balile amesema kuwa tume hiyo imebaini makosa kadhaa ya kisheria na uingiliaji wa taaluma yaliyofanywa na mkuu huyo wa mkoa na kupendekeza achukuliwe hatua.

Mkuu huyo wa mkoa hajajitokeza kujibu madai dhidi yake.