UGANDA

Asan Kasingye ateuliwa kuwa msemaji mpya wa jeshi la Polisi nchini Uganda

Maafisa wa Polisi nchini Uganda
Maafisa wa Polisi nchini Uganda Wikipedia

Inspekta Mkuu wa Polisi nchini Uganda Jenerali Kale Kayihura amemteua Mkurugenzi wa kitengo cha Interpol nchini humo Asan Kasingye kuwa Msemaji mpya wa jeshi la Polisi nchini humo baada ya kuuawa kwa Andrew Felix Kaweesi jijini Kampala wiki iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Pamoja na uteuzi huo, Kasingye pia ameteuliwa kuongoza idara ya kisiasa katika jeshi hilo la Polisi.

Marehemu Kaweesi ambaye alizikwa siku ya Jumanne wiki hii, amekuwa akisifiwa kama afisa aliyefanya kazi yake kwa kujitolea na kwa weledi wa hali ya juu.

Mbali na hayo, jeshi la polisi nchini humo linaendelea na operesheni ya kuwasaka wauaji wa Kaweesi.

Jenerali Kaihura tayari amesema washukiwa watatu wameshakamatwa baada ya kujaribu kuingia nchini DRC.

Serikali ya Uganda imesema itahakikisha kuwa wale wote waliotekeleza mauaji hayo watakamatwa na kuchukuliwa hatua.