TANZANIA

Rais Magufuli amfuta kazi Waziri wake wa Habari Nnape Nauye

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, amemfuta kazi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini humo Nape Nnauye.

Nnape Nauye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania
Nnape Nauye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania Wikipedia
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya Waziri huyo wa zamani kupokea ripoti kutoka kwa timu aliyoiunda kuchunguza hatua ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kuvamia kituo cha Habari cha Clouds akiwa na maafisa wa usalama waliojihami.

Ikulu ya Dar es salaam imetuma taarifa kwa vyombo vya Habari nchini humo kueleza hatua hiyo bila ya kutoa ufafanunuzi wa kina.

Nafasi ya Nape sasa imechukuliwa na Harrison George Mwakyembe ambaye awali alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Kufutwa kazi kwa Nape kumezua mjadala mkubwa nchini humo hasa katika mitandao ya kijamii wengi wakishutumu hatua hiyo.

Hata hivyo, Katiba ya Tanzania inampa mamlaka rais kuteua na kutengua uteuzi wa Mawaziri nchini humo.

Akizungumza mapema mapema wiki hii, rais Magufuli aliwashutumu wale wanaokosoa uongozi wake kupitia mitandao ya kijamii na kusema hakuna anayeweza kumwambia la kufanya kama kiongozi wa nchi.