Rais wa Somalia akutana na rais Kenyatta kujadili uhusiano wa nchi hizo mbili
Imechapishwa:
Rais mpya wa Somalia Mohamed Abdullahi anazuru nchi jirani ya Kenya, ikiwa ndio ziara yake ya kwanza nje ya nchi yake tangu alipochaguliwa mwezi Februari.
Rais huyo anayefahamika kwa jina maarufu la Farmajo, amekuwa katika Ikulu ya Nairobi na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake rais Uhuru Kenyatta.
Viongozi wa nchi hizo mbili wamekubaliana kuendeleza kushirikiana katika nyanya mbalimbali hasa suala la usalama na uchumi na uhusiano wa karibu kati ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Kenya imekuwa katika mstari wa mbele kuisaidia Somalia kuimarisha usalama wake na kupambana na kundi la kundi la kigaidi la Al Shabab.
Mbali na hilo, Kenya imekuwa kimbilio la maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia wanaopewa hifadhi katika kambi ya Daadab.
Kumekuwa na jaribio la Kenya kutaka kuwarudisha wakimbizi hao nchini Somalia kwa sababu za kiusalama lakini Mahakama mapema mwaka huu ilisema uamuzi huo ni kinyume cha Katiba.
Ziara hii imekuja wakati huu viongozi wa muungano wa IGAD wakitarajiwa kukutana siku ya Ijumaa, kujadili namna ya kushughulikia suala la wakimbizi wa Somalia.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa wakimbizi wa Somalia wapatao Milioni 2 wameyakimbia nchi yao.