KENYA

Magavana nchini Kenya wasema Madaktari hawatalipwa mshahara kwa muda waliogoma

Magavana nchini Kenya wamesema hawatawalipa Madaktari mshahara wao kwa muda wa miezi mitatu waliokuwa wamegoma.

Madaktari walio katika mgomo nchini Kenya wanomba nyongeza ya mshahara ya 50% kama ilivyokubaliwa katika mkataba uliosainiwa mwaka 2013.
Madaktari walio katika mgomo nchini Kenya wanomba nyongeza ya mshahara ya 50% kama ilivyokubaliwa katika mkataba uliosainiwa mwaka 2013. © Getty Images
Matangazo ya kibiashara

Madaktari nchini humo wanasema kuwa serikali za Kaunti zinastahili kuwalipa mshahara wao ambao kwa pamoja ni Shilingi za nchi hiyo Bilioni 3.2.

Magavana hao wanasema kuwa, hawakubaliana popote na Madaktari waliogoma kuwa watalipwa mshahara kwa kipindi walichokuwa wamegoma.

“Hatukuwahi kukubaliana kuwa tutawalipa Madaktari kwa muda waliogoma,” amesema Mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini humo Peter Munya.

Viongozi wa chama cha Madaktari nchini Kenya, wamesisitiza kuwa walikubaliana na serikali za Kaunti kuwa watalipwa mshahara wao wakati walipotia saini mkataba wa kurudi kazini.

Madaktari hao wametishia kuchukua hatua ambayo hawajaiweka wazi, ikiwa serikali za Kaunti hazitakubali kuwalipa mshahara wao kufikia wiki ijayo.