TANZANIA

Tanzania: Rais Magufuli awaonya wamiliki wa vyombo vya Habari

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli Screenshot/Azama TV

Rais wa Tanzania John Magufuli amewaonya wamiliki wa vyombo vya Habari nchini humo kwa kile alichosema, baadhi ya vyombo vya Habari nchini humo vinatangaza na kuandika Habari za uchochezi.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika Ikulu ya Dar es salaam siku ya Ijumaa, Magufuli amewashtumu baadhi ya wanahabari nchini humo kuandika taarifa ambazo amezitaja ni za kichochezi.

“Nawaambia wamiliki wa vyomvbo vya habari, be careful, watch, kama mnafikiri mna freedom ya namna hiyo, not to that extend,” alisema rais Magufuli.

Kiongozi huyo ameonekana kukerwa na taarifa zilizoandikwa katika Magazeti nchini humo zikionesha kutishiwa bastola dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Habari Nape Nnauye siku ya Alhamisi jijini Dar es salaam alipokuwa anataka kuzungumza na wanahabari.

“Picha yote ya ukurasa wa kwanza ni ya mtu aliyefanya kosa moja, kana kwamba hiki kitendo kimefanywa na serikali au kinaungwa mkono na serikali,” aliongeza rais Magufuli.

Aidha, amemwambia Waziri Mpya wa Habari Harrisson Mwakyembe kuhakikisha kuwa anachukua hatua pale ambapo mtangulizi wake alishindwa kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wanabahari nchini humo kuandika Habari zilizo sahihi na za usawa ili kuepusha ripoti zinazoweza kuzua uchochezi.