KENYA

Wanamgambo 31 wa Al-Shaabab wauawa na majeshi ya Kenya nchini Somalia

Wanajeshi wa Kenya  nchini Somalia
Wanajeshi wa Kenya nchini Somalia AFP/AU-UN/Stuart Price

Jeshi la Kenya limesema limewauwa magaidi 31 wa Al Shabab baada ya kuvamiwa kambi yao katika eneo la Baadhade, nchini Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi hilo Kanali Joseph Owuoth amesema pamoja na mauaji hayo, wamefanikiwa kupata silaha kadhaa ikiwa ni pamoja na bunduki 11 aina ya AK 47, vilipuzi na vifaa vya mawasiliano.

Mbali na vifaa hivyo, chakula na sare za kijeshi zimepatikana katika kambi hiyo.

KDF inayoshirikiana na mataifa mengine ya Afrika chini ya mwavuli wa AMISOM, inasema ilifanikiwa kutekeleza operesheni hiyo ikitumia ndege zake za kivita mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufanya msako dhidi ya magaidi hao.

Kanali Owouth ameongeza kuwa wapiganaji wengine wa Al Shabab walitoroka wakiwa na majeraha mabaya.

Mwaka 2011, serikali ya Kenya ilituma jeshi lake nchini Somalia kuungana na wanajeshi wengine kutoka barani Afrika kupambana na Al Shabab.

Licha ya mafanikio makubwa dhidi ya kundi la Al Shabab, ndani ya miaka miwili jeshi la Kenya limepoteza idadi isiyofahamika ya wanajeshi wake baada ya kuvamiwa na Al Shabab katika mashambulizi ya kushtukiza.

Mwezi Januari mwaka 2016 wanajeshi zaidi ya 100 waliuawa baada ya kushambuliwa na Al Shabab katika kambi yao ya El Adde na kuendelea kuwa shambulizi baya zaidi dhidi ya jeshi la Kenya tangu nchi hiyo ilipota uhuru wake mwaka 1963.