RWANDA

Mahakama Rwanda yaagiza kuachiwa kwa mke wa mwanasiasa anayeishi uhamishoni

Baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi nchini Rwanda wakiwa mahakamani hivi karibuni
Baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi nchini Rwanda wakiwa mahakamani hivi karibuni Stephanie AGLIETTI / AFP

Mke wa mwanasiasa wa upinzani wa Rwanda anayeishi uhamishoni nchini Uingereza na ambaye juma hili alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za makosa ya uhaini kwenye mahakama ya Kigali, mawakili wake wanasema mteja wao ataachiwa huru.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama imeagiza Violette Uwamahoro mwenye uraia wa Rwanda na Uingereza aachiwe huru, uamuzi unaoonekana kama pigo kwa waendesha mashtaka wa Serikali wanaojaribu kumshtaki kwa tuhuma za kuanzisha kundi la uasi, amesema wakili wake Antoinette Mukamusoni.

Shirika moja la kutetea haki za binadamu nchini humo linasema kuwa, jaji anayesikiliza kesi hiyo amegundua kuna mkanganyiko mkubwa kwenye ushahidi wa upande wa Serikali.

Hata hivyo Uwamahoro bado ameendelea kusalia kizuizini kwakuwa Polisi bado hawajapata nakala kutoka mahakama kuu.

Ikiwa Uwamahoro ataachiwa huru bado hatoruhusiwa kutoka nje ya mipaka ya Rwanda.

Waendesha mastaka wa Serikali wanazo siku 5 za kukata rufaa kupinga kuachiwa kwake huru na pia wanazo siku 30 kuamia ikiwa waendelee na kesi au waifunge ambapo baadae Uwamahoro ataachiwa bila ya masharti.

Upande wa mashtaka haujaonesha nia yoyote ikiwa unataka kuendelea na kesi hiyo au la.

Uwamahoro ambaye alichukua uraia wa Uingereza mwaka 2004 ambako anaishi na mume wake na watoto wawili, anatuhumiwa sambamba na binamu yake Jean-Pierre Shumbusho.

Kwa upande wake Shumbusho amekiri mashtaka yanayomkabili kwa kutoa siri za usalama wa nchi na kupanga kuunda kundi la wapiganaji kushambulia Rwanda lakini Uwamahoro anakanusha kushirikiana nae.

Uwamahoro ameolewa na mwanasiasa Faustine Rukundo, mwanasiasa wa chama cha RNC ambacho kiliundwa na washirika wa zamani wa rais Paul Kagame, Serikali ya Kigali inasema chama hicho ni mtandao wa kigaidi.

Uwamahoro alisafiri kwenda nchini Rwanda kuhudhuria mazishi ya baba yake lakini baadae akapotea kwenye mazingira ya kutatanisha Februari 14 ambapo Polisi walikiri kumshikilia majuma mawili yaliyopita wakisema anatuhumiwa kwa makosa ya uhaini.