CHINA

Bei ya pembe za ndovu yashuka bei nchini China

Sehemu ya shehena ya pembe za ndovu zilizochomwa hivi karibuni nchini Kenya.
Sehemu ya shehena ya pembe za ndovu zilizochomwa hivi karibuni nchini Kenya. REUTERS/Thomas Mukoya/File Photo

Bei ya pembe za ndovu imeshuka kwa theluthi mbili kwa muda wa miaka mitatu iliyopita nchini China.

Matangazo ya kibiashara

Utafiti uliofanywa na watalaam kutoka Shirika la kuhifadhi Wanyamapori la  Save the Elephants, umeonesha kuwa bei ya Kilo moja ya pembe za ndovu sasa ni Dola za Marekani 730 kutoka Dola 2,100.

Watalaam hao Esmond Martin na Lucy Vigne wamesema kushuka kwa bei hiyo ni habari njema sana katika vita dhidi ya uwindaji haramu hasa ndovu barani Afrika.

Aidha, inaelezwa kuwa hali hii imechangiwa pakubwa na kuonekana kutokuwa na uhitaji mkubwa wa pembe hizo za ndovu baada ya serikali ya China hivi karibuni kupiga marufuku biashara hiyo.

Sonia Riziki kutoka Ofisi ya Mawasiliano ya Shirika la Save the Elephants jijini Nairobi nchini Kenya, ameimbia RFI Kiswahili kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya licha ya bei hii kushuka lakini inatoa matumaini ya kufanikiwa kuwalinda ndovu barani Afrika.

Utafiti huu unakuja wakati huu kukiwa na hofu ya kutoweka kabisa kwa ndovu barani Afrika kwa sababu ya uwindaji haramu unaoendelea hasa nchini Kenya na Tanzania, eneo la Afrika Mashariki.

Idadi ya ndovu imeshuka barani Afrika kutoka ndovu 450,000 hadi 110,000 kwa muda wa miaka 10 iliyopita.

Biashara ya pembe za ndovu ilipigwa marufuku kimataifa mwaka 1989 lakini licha ya hatua hiyo biashara hiyo bado inaendelea na kuhatarisha uhai wa Wanyama hao.