Sweden yasema iko tayari kuongoza mazungumzo ya kisiasa nchini Uganda
Serikali ya Sweden imethibitisha kuombwa kuongoza mazungumzo ya kisiasa kati ya rais wa Uganda Yoweri Museveni na mpinzani wake wa siku nyingi Kizza Besigye pamoja na wadau wengine wa siasa nchini humo.
Imechapishwa:
Wizara ya Mambo ya nje nchini Sweden imeliambia Gazeti la kila siku nchini Uganda la Daily Moniter kuwa, nchi yake iko tayari kusaidia viongozi hao kuja katika meza ya mazungumzo ya kumaliza tofauti zao.
Msemaji wa Wizara hiyo Katarina Byrenius Roslund, amesema nchi yake ina uzoefu wa utatuzi wa migogoro na uhimizaji amani, na itakuwa katika nafasi nzuri ya kufanikisha mazungumzo hayo.
Kumekuwa na wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa nchini humo hasa kati ya rais Museveni na Besigye ambao wamekuwa wapinzani na kuzua wasiwasi wa kisiasa nchini humo.
Baada ya Uchaguzi mwaka 2016, ambao rais Yoweri Museveni alitangazwa mshindi na Besigye kulalamikia vikali matokeo hayo, kumekuwa na wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa nchini humo.
Besigye amekuwa akisema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo hayo lakini akitoa sharti kuwa yaongozwe na msuluhishi kutoka nje ya nchi.
Moja ya suala nyeti la kujadiliwa katika mazungumzo hayo ikiwa yatafanyika ni rais Museveni kuendelea kukaa madarakani kwa muda mrefu.