SUDAN KUSINI

Machar atakiwa kuwaagiza waasi wake kuacha vita nchini Sudan Kusini

Riek Machar ( Kushoto) akiwa na rais wa zamani wa Bostwana  Festus Mogae, mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Afrika Kusini
Riek Machar ( Kushoto) akiwa na rais wa zamani wa Bostwana Festus Mogae, mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Afrika Kusini Moniter

Mwenyekiti wa Kamati inayothathmini utekelezwaji wa mkataba wa amani nchini Sudan Kusini na rais wa zamani wa Bostwana Festus Mogae, anamtaka kiongozi wa waasi Riek Machar kutangaza usitishwaji wa mapigano kati ya vikosi vyake na wanajeshi wa serikali.

Matangazo ya kibiashara

Mogae ametoa wito huo baada ya kukutana na Machar mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Afrika Kusini anakoishi kwa sasa baada ya kuondoka nchini Juba mwaka 2016.

Msemaji wa Machar, Lam Kuei Lam amethibitisha kufanyika kwa mkutano huo na kuongeza kuwa pamoja na wito huo, Mogae amemtaka Machar kukubali kuja katika meza ya mazungumzo ya kitaifa na rais Salva Kiir.

Ripoti zinasema kuwa Machar ameonekana kukubali ombi hilo baada ya rais Kiir naye kuwaambia marais kutoka ukanda wa IGAD kusema kuwa atatangaza usitishwaji wa vita dhidi ya waasi kote nchini.

Sudan Kusini imekosa amani licha ya kusainiwa kwa mkataba wa amani mwaka 2015 kati ya rais Kiir na Machar jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Rais Kiir amekuwa akisema yuko tayari kuzungumza na Machar ili kupatikana kwa amani ya kudumu katika taifa hilo changa duniani.