KENYA-SIASA

Upinzani nchini Kenya kumtaja mgombea wake wa urais

Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya  Musalia Mudavadi, Raila Odinga, Issac Ruto, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula
Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Musalia Mudavadi, Raila Odinga, Issac Ruto, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula todayonline.

Maelfu ya wafuasi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, wamefurika katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi kusubiri tangazo la mgombea urais kupitia muungano huo.

Matangazo ya kibiashara

Wanaowania tiketi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, aliyekuwa Makamu wa rais Kalonzo Musyoka, Seneta Moses Wetangula na Musalia Mudavadi.

Wanasiasa hao wamekuwa wakikutana kwa kipindi cha miezi kadhaa ijayo, kuona ni upi kati yao anaweza kupambana na rais Uhuru Kenyatta wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti mwaka huu.

Wiki iliyopita, wanasiasa hao waliwaambia wafuasi wao kuwa tayari wameshakubaliana ni nani kati yao atapeperusha bendera ya muungano huo.

Uchaguzi wa mwaka 2013, muungano mwingine wa upinzani uliofahamika kama CORD, uliongozwa na Raila Odinga kama mgombea wake na Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini humo wamekuwa wakisema kuwa, huenda mpangilio wa mwaka 2013 ukarudiwa tena huku wengine wakisema huenda mabadiliko yakafanyika.