KENYA-SIASA

Chama cha ODM chamwidhinisha Odinga kuwania urais kupitia muungano wa NASA

Mgombea wa urais nchini kupitia muungano wa upinzani NASA  Raila Odinga
Mgombea wa urais nchini kupitia muungano wa upinzani NASA Raila Odinga REUTERS/Thomas Mukoya

Wajumbe wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya cha ODM, wamemwidhinisha Raila Odinga kuwania urais kupitia muungano wa upinzani NASA.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja wiki moja baada ya Odinga ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, kupewa tiketi ya muungano wa NASA kupambana na rais Uhuru Kenyatta wakati wa uchaguzi Mkuu tarehe 8 mwezi Agosti.

Imekuwa ni mara ya  tatu kwa chama cha ODM, kumwidhinisha Odinga kuwania urais, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2007 na 2013.

Kalonzo Musyoka mgombea mwenza wa Odinga amesema kuwa, upinzani hautakubali tena wizi wa kura kama ilivyofanyika miaka iliyopita.

Aidha, ametoa wito kwa wafuasi wa upinzani kuhakikisha kuwa wanalinda kura zao ili kufikia mabadiliko ya NASA kuingia madarakani.

"Nitahakikisha kuwa mimi na Raila tunaunganisha taifa, tuache ukabila," alisema Kalonzo.

Nacho chama tawala cha Jubilee cha rais Uhuru Kenyatta kitakuwa na mkutano wake siku ya Jumamosi kumwidhinisha mgombea wake anayewania kwa muhula wa pili.

Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema kuwa kampeni rasmi zitaanza tarehe 30 mwezi huu kwa kipindi cha miezi mitatu.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema uchaguzi wa urais unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.