SUDAN KUSINI-UNICEF

Vita nchini Sudan Kusini vyasababisha watoto zaidi ya Milioni 1 kukimbia makwao

Baadhi ya wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa na watoto
Baadhi ya wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa na watoto Oxfam

Umoja wa Mataifa unasema watoto Milioni moja nchini Sudan Kusini wameikimbia nchi hiyo na wazazi wao kutokana na mapigano yanayoendelea.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la UNICEF linasema kuwa mtoto mmoja kati ya watano nchini Sudan Kusini wameyakimbia makwao.

Watoto ni asilimia 62 ya wakimbizi wapatao Milioni 1.8 waliokimbia nchini Uganda, Kenya, Ethiopia na Sudan.

Mkuu wa UNICEF barani Afrika Valentin Tapsoba, amesema kuwa hali ya wakimbizi ni mbaya sana nchini Sudan Kusini.

Mbali na wakimbizi hao, watoto wengine zaidi ya 1,000 wameuawa au kujeruhiwa katika mapigano yanayoendelea mwaka 2013.

Pamoja na hilo, robo tatu ya wanafunzi wote nchini humo hawaendi shuleni kwa sababu ya mapigano yanayoendelea.

Kumekuwa na jitihada kutoka Jumuiya ya Kimataifa kwa rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar kuagiza vikosi vyao kuacha mapigano, juhudi ambazo hazijazaa matunda.